Jumamosi 4 Julai 2026 - 11:20
Serekali Imefanya Mapinduzi Dhidi ya Katiba; Muqawama Utaendelea Muda wa Kuwa Uvamizi Huu Upo

Hawza / Mustafa Bairam amesema: Dola ya Lebanon imejisalimisha kwa kutia saini kile alichokiita "makubaliano ya fedheha na aibu yaliyoandikwa na Benjamin Netanyahu."

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Mustafa Bairam, Waziri wa zamani wa Lebanon, alisema katika hotuba yake kwenye hafla ya kuwaenzi mashahidi iliyofanyika katika mji wa Jbaa, kwamba utawala wa Lebanon umejisalimisha kwa kutia saini kile alichokiita "makubaliano ya fedheha na aibu yaliyoandikwa na Benjamin Netanyahu."

Alisisitiza kuwa; jukumu la utawala limebakia katika "kutia saini kwa fedheha" pekee, ilhali Iran ndiyo iliyowezesha kusitishwa kwa mapigano na kuiweka Lebanon katika kifungu cha kwanza cha makubaliano hayo; si kwa ajili ya kujadili kifungu hicho, bali kukiweka chini ya mwavuli wa ulinzi hadi pale Walebanon watakapofanya mazungumzo kuhusu kuondoka kwa vikosi vya uvamizi. Hata hivyo, utawala ulikataa jambo hilo kwa sababu ulidhani kwamba adui wa pamoja wa Lebanon na Israel ni Muqawama.

Bairam alihoji: "Katiba iko wapi? Sheria ya Lebanon iko wapi?" Akabainisha kwamba Katiba ya Lebanon inaitambua Israel kuwa ni adui na inarejea kwenye Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaohakikisha haki ya mataifa kujitawala. Aidha, Hati ya Maridhiano ya Kitaifa pamoja na Mkataba wa Haki za Binadamu wa Kiarabu vinathibitisha haki ya kupambana na uvamizi, ilhali sheria ya Lebanon inaharamisha na kuifanya kuwa kosa la jinai aina yoyote ya mahusiano au ushirikiano na Israel.

Aliongeza kuwa; utawala umeipindua Katiba, umeivunja sheria na makubaliano ya kitaifa, umeufanya Muqawama kuwa mhalifu katika ardhi yake yenyewe, na umechukua uamuzi wa Kizayuni unaohalalisha kuendelea kuwepo kwa vikosi vya uvamizi na kuendelea kwa mashambulizi yao.

Waziri huyo wa zamani wa Lebanon alisisitiza kwamba; kama ambavyo saini hiyo ya fedheha itafutika, ndivyo pia utawala wa Kizayuni utakavyotoweka, na kila atakayejifungamanisha na mradi wa Kizayuni ataondoka pamoja nao. Alisisitiza kuwa Muqawama hautafanya kazi kwa mujibu wa matakwa ya Israel, bali utaendelea kushikamana na mambo mawili: mkono wake utaendelea kuwa juu ya kichocheo cha silaha, na katika ardhi ambayo Muqawama ipo, hakutakuwa na uvamizi wowote utakaobaki. Aidha, kipaumbele cha kifungu cha kwanza katika maelewano kati ya Iran na Marekani ni kulinda mamlaka ya kitaifa na usalama wa Lebanon.

Bairam alisema kwamba; kile kilichofanywa na utawala ni usaliti dhidi ya Katiba, ni pigo kwa Makubaliano ya Taif, kwa maridhiano ya kitaifa na kwa haki za mataifa, na ni mapinduzi dhidi ya kujitolea mhanga na maslahi ya wananchi. Aliutaja utawala ambao hauwakilishi maumivu na matumaini ya wananchi wa Lebanon kuwa ni "utawala ulioanguka na wa mpito."

Aliongeza kuwa; Katiba inabainisha wazi kwamba wananchi ndio chimbuko la mamlaka yote, na utawala ni wakala wao tu. Hivyo basi, iwapo utawala huo utasaliti dhamana yake na kuachana na mamlaka ya kitaifa, wananchi watarejesha mamlaka hiyo mikononi mwao na wataondoa uhalali kwa yeyote asiyeustahili.

Bairam alihitimisha kwa kusema: Wote ni wenye kupita na kutoweka, lakini Lebanon itaendelea kuwa nchi yenye heshima na hadhi kwa watu wote waaminifu kutoka katika madhehebu na mielekeo mbalimbali, nguvu yetu kuu ni umoja wetu, na nguvu yetu kuu ni Muqawama wetu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha